Kurasa

Jumanne, 9 Juni 2015

KATIBA YA MTANDAO WA MARAFIKI WA ELIMU GEITA YAPATIKANA

HATIMAYE MARAFIKI WA ELIMU WA WILAYA YA GEITA WANAOUNDA MTANDAO WA MARAFIKI WA ELIMU WILAYA GEITA (FENGD) WAMEFANIKIWA KUPITISHA KATIBA YAO HAPO JUMA MOSI YA TAREHE 06/06/2015 KATIKA KITUO CHA WALIMU KATORO



KATIBA YA MARAFIKI WA ELIMU (W) GEITA (FENGD),

TOLEO LA KWANZA 2015.

SEHEMU YA KWANZA:

1: UTANGULIZI:

IBARA YA 1: UTANGULIZI:

Sisi Marafiki wa Elimu wilaya Geita  {Friends Of Education Network Geita District} (FENGD) ambao ni muunganiko wa wanachama wa harakati za marafiki wa elimu waishio katika wilaya ya  Geita; kwa hiari yetu tumeamua kujiunga kisheria ilil kushughulikia masuala ya kuboresha  Elimu, Demokrasia, Utawala bora na mawasiliano katika jamii ya Geita kwa kushirikiana na wananchi wa kada zote na wadau mbalimbali.

Asasi hii imeanzishwa kwa matakwa ya wanaharakati wenyewe kwa lengo la kujihusisha  na kuelimisha jamii ili kuboresha elimu na demokrasia bila shinikizo toka kwa wana siasa, vikundi vya dini au ukabila. Asasi hii itatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria za nchi kanuni na taratibu za mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Tanzania.

IBARA YA 2: JINA LA KATIBA NA KUANZA KUTUMIKA:

2:1 Jina la Katiba.

Katiba hii ni  waraka halali wa FENGD, hivyo itajulikana na kutambulika kwa jina la katiba ya “Marafiki wa Elimu (w) Geita (FENGD)”

           

2:2 Tarehe rasmi ambayo katiba hii itaanza kutumika.

Katiba hii itaanza kutumika mara baada ya kupata usajli rasmi na wanachama wa FENGD kufanya uchaguzi wa viongozi kwa mujibu wa katiba hii.

 

IBARA YA 3: LUGHA YA ASASI:

Kwa kuwa FENGD ni asasi huru yenye wanachama wenye viwango tofauti vya elimu; na kwakuwa FENGD inafanya kazi na watu wa kada tofauti: lugha kuu ya mawasiliano itakuwa Kiswahili na lugha ya pili itakuwa Kiingereza

 

SEHEMU YA PILI:

 

SEHEMU YA II: KATIBA, USAJILI, ANUANI YA OFISI NA ENEO LA UTENDAJI KAZI:

 

IBARA YA 4: Katiba

            Katiba ya FENGD ndio muongozo wa shughuli zote za Asasi hii.

 

IBARA YA 5: Jina la Asasi  

            Asasi hii itaitwa MTANDAO WA MARAFIKI WA ELIMU (W) GEITA kwa kifupisho FENGD.

 

 

IBARA YA 6: Usajili na Anuani

6:1       Baada ya kusajiliwa; makao makuu ya FENGD yatakuwa katka eneo lolote wilayani Geita katika Jamhuriya Muungano wa Tanzania kulingana na makubaliano ya wanachama.

 

6:2       Anuani ya FENGD itakuwa:-

            Mtandao wa Marafiki wa Elimu Geita,

            S.L.P 45, Geita.

 

IBARA YA 7: Eneo la utendaji kazi

            FENGD itafanya kazi katika mkoa wa Geita kwa kuhusisha ngazi mbalimbali za uanachama za FENGD.

 

IBARA YA 8: Washirika wa FENGD.

            FENGD itakuwa na haki ya kushirikiana na Taasisi, Mashirika mbalimbali ndani na nje ya Tanzania, watu binafsi, makampuni na Asasi nyingine ambazo zitakkuwa na nia ya  kusaidia na kushirikiana na FENGD katika kutekeleza Dira na Dhamira ya FENGD.

 

IBARA YA 9: Kanuni za Kimaadili.

9:1    Katika kutekeleza majukumu yake; FENGD itazingatia maadili, uadilifu, nidhamu, uwajibikaji kujituma kujitolea na uchapakazi kwa manufaa ya taifa.

9:2       Wanachama na viongozi wa FENGD lazima wawe waadilifu.

 

 

SEHEMU YA 3:

 

SEHEMU YA III: DIRA, DHAMIRA, MADHUMUNI NA ULINZI WA ASASI:

 

IBARA YA 10: Dira ya FENGD:

Nikuwa na Geita yenye mazingira bora ya elimu, utawala bora, Demokrasia ya kweli kwa wananchi wote mfumo bora na imara wa mawasiliano ndani ya jamii.

 

IBARA YA 11: Dhamira ya FENGD

Kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusiana na chamngamoto za elimu, Demokrasia na Utawala bora na namna ya kushirikiana na serikali na jamii kuzikabili changamoto hizo ilil kuleta mafabnikio chanya kwa manufaa ya umma.

 

IBARA YA 12: Madhumuni ya FENGD.

12:1   Kufanya ufatiliaji na uchambuzi wa masuala ya elimu, demokrasia, utawala bora na kuimarisha mfumo wa mawasiliano katika jamii na vyombo vya utawala.

12:2   Kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa ushiriki wao katika mikutano kwa manufaa ya kijamii na kukabiliana na changamoto za maendeleo katika maeneo yao

12:3   Kuendesha midahalo, mikutano, mijadala, na makongamano ya kijamii juu ya masuala mbalimbali na kukabiliana na changamoto za maendeleo.

12:4   Kutumia vyombo vya habari kama redio, TV na magazeti kuelimisha jamii

12:5   Kujihusisha kikamilifu katika kusaidia jamii kitaaluma na ushauri katika masuala yanayo kwamisha maendeleo yao

12:6     Kutoa elimu kwa jamii hususani vijana wa shule za Msingi, Sekondari na vyuo pamoja na walio nje ya shule kuhusiana na haki zao za msingi, elimu ya afya ya uzazi, elimu kuhusiana na VVU/UKIMWI, magonjwa ya ngono, madhara ya matumizi ya dawa za kulevya, elimu ya ujasiriamali na kuinua kipato, pamoja na masuala  mtambuka kama mazingira n.k.

12:7     Kutoa elimu ya Demokrasia na Utawala bora na Usawa wa kijinsia katika jamii.

12:8     Kuanzisha club za Marafiki wa Elimu ndani na nje ya shule za msingi, sekondari na vyuo kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali ya elimu, demokrasia na utawala bora katika jamii.

 

IBARA YA 13: ULINZI WA ASASI:

            Asasi hii itatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria zilizowekwa na serikali ya jamhuri ya muungano wa Tanzania; na dhamira  yake ya kutekeleza shughuli zake kwa mujibu wa katiba yake na sheria za Tanzania.

 

SEHEMU YA 4:

 

SEHEMU YA IV: AINA ZA UANACHAMA WA FENGD:

 

IBARA YA 14: UANACHAMA.

            Kutakuwa na aina tatu tu za uanachama wa FENGD kwa mujibu wa katiba hii ambazo ni;

 

            14: 1    Wanachama  waanzilishi.

            14.1.1  Huu ni uanachama wa watu walishiriki katika kuanzisha wazo la kuundwa kwa

FENGD na ambao kwa namna moja au nyingine walifanikisha FENGD kupata usajili.

 

            14:2     Wanachama binafsi

            14.2.1  Huu ni uanachama wa mtu binafsi ambaye kwa mapenzi yake atapendezwa na

shughuli za FENGD na kuamua kujiunga kuwa mwanachama kwa hiari yake

mwenyewe.

            14.2.2  Kwa mujibu wa katiba hii, kuwa mwanachama wa FENGD katika wilaya

hakuunyimi kuwa mwanachama mkoa wala Taifa.

 

            14.3     Uanachama wa Heshima

            14.3.1  Mtu binafsi, shirika, kampuni au Taasisi yoyote wanaweza kuwa wanachama wa

FENGD kwa kuchaguliwa /kuteuliwa na kamati kuu ya uongozi ya FENGD kisha

kuandikiwa barua ya nia hiyo na iwapo watakubali watakuwa wanachama rasmi wa FENGD.

            14.3.2  Mwanacham wa heshima wa FENGD hatapiga kura ya maamuzi juu ya jambo lolote

linalohusu FENGD.

 

IBARA YA 15: SIFA ZA MWANACHAMA:

            15:1     Wanachama waanzilishi watatambuliwa kwa sifa zifuatazo:

            15.1.1  Awe ni mtu aliyejitolea kwa hali na mali katika kuanzishwa kwa FENGD

            15.1.2  Awe na nia ya dhati ya kuhakikisha kuwa atakuwa mstari wa mbele kutimiza

Dira na Dhamira ya FENGD.

            15.1.3  Atambue kuwa anapaswa kuitumikia FENGD na si FENGD imtumikie

            15.1.4  Awe tayari kushirikiana na wadau wengine ili kulinda maslahi ya taifa

 

            15.2     Mwanachama binafsi

            15.2.1  Awe ni mtu mwenye kuziunga mkono kwa dhati shughuli na juhudi za FENGD

            15.2.2  Awe mwenye kujitoa kuitetea FENGD ili kufanikisha malengo yake

            15.2.3  Awe na uwezo wa kuisaidia FENGD kwa hali na mali pasipo kuchoka

            15.2.4  Awe mtu yeyote mwenye akili timamu na umri usiopungua miaka mitano (5)

 

IBARA YA 16: HAKI ZA MWANACHAMA

                        Wanachama wa FENGD wana haki zifuatazo.

           

            16.1     Kuhudhuria vikao vinavyo wahusu kwa mujibu wa katiba hii

            16.2     Kupata taarifa ya FENGD kwa kufuata taratibu zilizopo

  16.3   Kushiriki katika vikao mbalimbali vya maamuzi ya FENGD kwa mujibu wa taratibu

            16.4     Kuchaguliwa au kuchagua viongozi wa FENGD kwa mujibu wa wa taratibu za

Katiba.           

            16.5     Haki ya kujitetea na kujieleza kwa tuhuma/kosa alilotenda mbele ya vyombo vya

FENGD.

            16.6     Haki ya kuteuliwa kuiwakilisha FENGD katika maeneo/ shughuli mbalimbali

            16.7     Haki ya kupata taarifa na kuzitumia kwa manufaa ya FENGD na jamii.

16.8       Haki ya kushiriki na kushirikisha uongozi na wanachama wa FENGD katika mambo yenye manufaa kwa FENGD na jamii.

16.9     Haki ya kuwa na nakala ya katiba ya FENGD

 

 

IBARA YA 17: WAJIBU WA MWANACHAMA:

                        Wajibu wa mwanachama wa FENGDni pamoja na:,

            17.1     Kulipa ada na michango yote ya FENGD kwa ajili ya uendelevu wa Asasi

            17.2     Kuhudhulia vikao na mikutano yote inayohusu kwa mujibu wa katiba hii.

            17.3     Kuwa mwaminifu, mwadilifu mkweli na kutetea msimamo wa FENGD katika

Maendeleo.

            17.4     Kuchangia mawazo kwa hali na mali katika kulinda Dira na Dhamira ya FENGD.

            17.5     Kufahamu kwa undani katiba ya mtandao

 

IBARA YA 18: KUKOMA UANACHAMA:

                        Uanachama utakoma kwa:

            18.1     Mtandao wa wilaya kufutwa kwa mujibu wa sheria za nchi

            18.2     Mwanachama kuamua kujiudhulu kwa hiari yake

            18.3     Kufukuzwa uanachama

            18.4     Kushindwa kulipa ada kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo bila sababu za msingi

            18.5     Kukiuka maadili ya uanachama wa FENGD kwa makusudi

            18.6     Kwa kutenda kosa lolote ambalo wanachama wataridhia kwamba linafaa

kumuondoa katika uanachama wa FENGD na uamuzi huo kuridhiwa na mkutano

mkuu.

 

SEHEMU YA TANO:

 

SEHEMU YA V: MUUNDO NA WAJIBU WA VIONGOZI:

 

IBARA YA 19:    MUUNDO NA WAJIBU WA VIONGOZI:

                        Uongozi wa FENGD utakuwa kama ifuatavyo

 

            19.1     Mwenyekiti wa FENGD

            19.2     Makamu mwenyekiti wa FENGD

            19.3     Katibu wa  FENGD

            19.4     Mratibu wa FENGD

            19.5     Mweka hazina wa FENGD

 

            19.1.0  Mwenyekiti

                        Wajibu wa mwenyekiti utakuwa kama ifuatavyo:

 

            19.1.1  Mwenyekiti ataongoza Mikutano ya Bodi ya ushauri na mkutano mkuu wa

Wanachama

            19.1.2  Mwenyekiti atakuwa msemaji mkuu wa FENGD katika mikutano ya bodi ya ushauri

na mkutano mkuu wa wanachama

19.1.3  Aache hisia zake binafsi zikiangalia maamuzi ya wengi ila pale kunapokuwa na usawa wa maamuzi kwa pande mbili.

 

            19.2.0  Makamu Mwenyekiti

            19.2.1  Makamu mwenyekiti atafanya kazi za mwenyekiti kama mwenyekiti hayupo

            19.2.2  Atafanya kazi za mwenyekiti kwa kuagizwa

 

            19.3.0  Katibu

                        Katibu atakuwa na kazi zifuatazo;

            19.3.1  Atatunza kumbukumbu za vikao vya bodi ya ushauri na mikutano ya FENGD

            19.3.2  Ndiye katibu wa mikutano ya kamati ya UBodi ya Ushauri na mkutano mkuu wa

FENGD.

            19.3.3  Katibu atawasiliana na mwenyekiti na makamu mwenyekiti kwa maamuzi ya

utekelezaji

            19.3.4  Kuandika barua na kuitisha vikao baada ya kuwasiliana na mwenyekiti

            19.3.5  Kuandaa agenda za mikutano ya Bodi ya Ushauri, Mkutano mkuu na mikutano ya

Dharula

            19.3.6  Kuandaa taarifa mbalimbali za FENGD na kuzipeleka pale zinapohitajika

 

            19.4     MRATIBU

            19.4.1  Kuratibu shughuli mbalimbali za kamati ndogo ndogo za FENGD

            19.4.2  Kuratibu shughuli zote za kila siku za FENGD

            19.4.3  Kufuatilia utekelezaji wa maamuzi ya mikutano ya bodi ya ushauri na mkutano

mkuu wa FENGD.

            19.4.4  Kushughulikia suala la utafutaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya uendelevu

wa FENGD

            19.4.5  Ndiye mkuu wa kitengo cha mawasiliano na utafiti

 

 

            19.5.0  Mweka Hazina

                        Mweka hazina atakuwa na wajibu ufuatao;

            19.5.1  Atakuwa mtunzaji mkuu wa fedha za FENGD

            19.5.2  Atasimamia utunzaji wa vitabu vya kumbukumbu za fedha za FENGD

            19.5.3  Ataandaa na kutoa taarifa za fedha za FENGD katika vikao vya Bodi ya Ushauri na

Mkutano mkuu wa FENGD.

            19.4.4  Atakuwa mdhamini wa mali za Asasi kwa niaba ya FENGD

 

 

SEHEMU YA SITA:

 

SEHEMU YA VI: BODI YA USHAURI, MAMLKA NA MIKUTANO:

 

IBARA YA 20:      BODI YA USHAURI

            20.0     Kuanzisha Bodi

                        Kutakuwa na bodi ya FENGD ambayo itajulikana kama “BODI YA USHAURI”

                        Bodi hii itaundwa na wajumbe tisa (9) na itadumu madarakani kwa muda wa

miaka mitatu (3) na inaweza kuchaguliwa tena kuendelea na majukumu yake kwa

si zaidi ya vipindi viwili.

            20.1     Wajumbe wa Bodi.

                        Bodi ya ushauri ya FENGD itakuwa na wajumbe kumi (10) ambao kati yao wanawake

watatu (3) wajumbe watapatikana kama ifuatavyo:

            20.1.1  Mwenyekiti wa FENGD

            20.1.2  Makamu mwenyekiti wa FENGD

            20.1.3  Mratibu ambaye pia ni Katibu wa FENGD

            20.1.4  Mweka hazina wa FENGD

            20.1.5  Wajumbe wawili (2) kutoka wanachama waanzilishi wa FENGD

            20.1.6  Wajumbe watatu (3) wa kuchaguliwa na mkutano mkuu wa FENGD

 

IBARA YA 21:  WAJIBU, MAMLAKA NA KAZI ZA BODI YA USHAURI

                        Bodi ya Ushauri itakuwa na kazi na mamlaka kama ifuatavyo:

            21.1.1  Itakuwa na mamlaka na madaraka ya kupokea tarifa za utekelezaji wa kazi za

FENGD

            21.1.2  Kutoa ushauri kwa uongozi na kutatua migogoro ndani ya FENGD

            21.1.3  Kufanya mapitio ya bajeti na kutoa maoni ya kuzingatiwa na watendaji wa FENGD

            21.1.4  Bodi ndio yenye mamlaka ya kuajiri watendakji wa FENGD

 

IBARA YA 22: MIKUTANO/VIKAO VYA FENGD NA MAJUKUMU YAKE.

                        FENGD Itakuwa na Mikutano/vikao kama ifuatavyo;

            22.1.0  Mkutano Mkuu

            22.1.1  Kutakuwa na mkutano mkuu wa wanachama ambao utafanyika mara moja kila

mwisho wa mwaka

            22.1.2  Mkutano utahudhuliwa na watendaji wote wa FENGD, wanachama hai (waliolipa

Kiingilio na ada), wanachama waanzilishi wa FENGD, wanachama wa heshima na

wageni mbalimbali watakao alikwa kuhudhulia

22.1.3  Mkutano mkuu ndio chombo chenye madaraka yote ya kuamua mambo muhimu ya FENGD ikiwa ni pamoja na kupitisha sera na taratibu mbalimbali za kusimamia uendeshaji wote wa Asasi

22.1.4  Kuchagua mwenyekiti, makamu mwenyekiti, mweka hazina, na wajumbe wa bodi ya ushauri ya FENGD pamoja na wajumbe wa kamati mbalimbali.

22.1.5  Kupokea na kupitisha makisio ya mapato na matumizi ya FENGD kutoka kwa muweka hazina.

22.1.6  Kupitisha jina la mkaguzi wa mahesabu ya FENGD

22.1.7  Kujadili na kupitisha taarifa za mwaka za utekelezaji wa shughuli za FENGD

22.1.8  Kujadili na kupitisha mabadiliko ya katiba ya FENGD

22.1.9  Kujadili na kupitisha mikakati yna mipango ya muda mfupi na mrefu ya FENGD

22.1.10Kufanya maamuzi yote ya FENGD, kama itakavyo onekana inafaa.

 

22.2.0  Mkutano Mkuu wa dharura

22.2.1  Mkutano wa dharura unaweza kuitishwa endapo kutakuwa na ombi lililotolewa na kutiwa saini na si chini ya theluthi mbili idadi ya wanachama na kuweka bayana katika ombi hilo suala ambalo limesababisha kuitishwa kwa mkutano mkuu wa dharura.

22.2.2  Mkutano Mkuu wa dharura utahudhuliwa na watendaji wote wa FENGD, wanachama hai (waliolipa ada na kiingilio), wanachama waanzilishi, wanachama wa heshima na wageni waalikwa.

            22.2.3  Mkutano Mkuu wa dharura unaweza kuitishwa mara moja tu (1) kwa mwaka.

 

            22.3.0  Bodi ya Ushauri

            22.3.1  Bodi hii itakuwa na madaraka ya kuongoza na kusimamia kazi zote za FENGD na

kazi zote zitakazo elekezwa na mkutano mkuu.

            22.3.2  Bodi hii itakuwa na madaraka ya kupitia taarifa za utendaji/ utekelezaji za katibu

kwa ajili ya kuziwasilisha kwenye mkutano mkuu

            22.3.3  Kuratibu na kuongoza kazi za kamati ndogondogo za FENGD na watendaji wake

            22.3.4  Kuandaa rasimu ya marekebisho ya katiba kwa ajili ya kujadiliwa na mkutano

Mkuu

            22.3.6  Kuandaa rasimu ya sera na taratibu mbalimbali kwa ajili ya kupelekwa kwenye

mkutano mkuu kwa uthibitisho

            22.3.7  Kuandaa rasimu ya mipango ya muda mfupi na muda mrefu na bajeti ya kila

mwaka kwa ajili ya utekelezaji wa shughuli za FENGD.

            22.3.8  Kuandaa agenda na kuhakikisha kuwa mkutano mkuu unafanyika kwa wakati

            22.3.9  Kuandaa kamati ndogondogo za maeneo maalumu ya utekelezaji.

            22.3.10Kuitisha mikutano ya Bodi na mkutano mkuu wa dharura si zaidi ya mara mbili tu

kwa mwaka kama kuna ulazima wa kufanya hivyo

22.3.11Kuandaa sheria ndogondogo na kanuni za FENGD.

 

SEHEMU YA SABA:

 

SEHEMU YA VII: UENDESHAJI WA MIKUTANO NA VIKAO VYA FENGD

 

IBARA YA 23: UENDESHAJI WA VIKAO:

 

23.1  Taarifa ya mkutano mkuu wa kawaida itatolewa kwa kila mwanachama si chini ya siku kumi na nne (14), na taarifa ya mkutano mkuu wa dharura itatolewa kwa wanachama si zaidi ya siku saba (7), kabla ya siku ya mkutano husika.

23.2  Wanachama watakaotaka kuleta mawazo/ agenda maalumu kwenye Mkutano Mkuu, watatoa taarifa ya maandishi kwa katibu wa FENGD siku saba kabla ya siku ya mkutano.

23.3  Nusu ya idadi ya wanachama halali wa mkutano mkuu watakamilisha akidi (Quorum) ya mkutano wowote ule isipokuwa kwamba akidi haitahitajika endapo Mkutano umetokana na mkutano ulioahirishwa; endapo wanachama watakao kuwepo watachukuliwa kutosheleza akidi.

23.4  Katika mkutano unaotokana na mkutano ulioahirishwa hautaruhusiwa kufanya maamuzi yoyote ya kubadili katiba ya FENGD.

23.5  Endapo saa moja na nusu itapita tangu muda uliokubaliwa kuwa ndio wa kuanza mkutano bila idadi ya wajumbe kutimia ili kuweza kufanya mkutano; basi mkutano uta ahirishwa na Mwenyekiti au makamu mwenyekiti hadi siku kama hiyo wiki inayofuata.

22.6 Mwenyekiti ndiye atakayeongoza mikutano ya Bodi, Kamati ya Utendaji, Mkutano Muu na Mkutano Mkuu wa dharura.

22.7  Makamu mwenyekiti ataongoza shughuli za mikutano kama mwenyekiti hayupo.

22.8 EndapoMwenyekiti na makamu mwenyekiti hawakuhudhulia basi mjumbe mmoja anaweza kupendekezwa kuwa mwenyekiti kwa wakati huo.

22.9  Katika mkutano mkuu maamuzi yatatokana na kupiga kura kwa kuinua mikono juu isipokuwa kama wanachama walioko katika mkutano wanamua kwamba kura zipigwe kwa siri (secret ballot).

22.10 Uamuzi utaonekena kuwa umepitishwa kwa idadi ya wingi wa kura kuunga mkono hata kama tofauti ni ya kura moja (Majority decision) isipokuwa kama kura ni kwa ajili ya  kubadili katiba basi kura ni lazima ziwe siyo chini ya theluthi mbili ya idadi ya wanachama waliohudhulia kukubali.

22.11   Hakutakuwepo na upigaji kura ya uwakilishi (no voting by proxy)

22.12 Katika upigaji kura endapo kura zitafungana Mwenyekiti atakuwa na kura ya Mwisho (Casting vote)

22.13   Ni budi Mwenyekiti aheshimiwe wakati wa mkutano

22.14   Uamuzi wa mwenyekiti katika kudhibiti mwenendo wa mkutano ni wa mwisho labda kama atapingwa na theluthi ya wajumbe.

22.15  Mwenyekiti anamamlaka ya kuingilia usumbufu wowote unaojitokeza wakati wa Mkutano au kumtoa nje mjumbe ambaye anasumbua mwenendo wa mkutano.

22.16   Mjumbe atakayetolewa nje kwa ajili ya usumbufu atatakiwa aondoke eneo la Mkutano.

           

 

SEHEMU YA NANE:

 

SEHEMU YA VIII: UCHAGUZI NA MUDA WA KUKAA MADARAKAN.

24.0     Muda wa Uongozi

24.1     Viongozi watakao chaguliwa kwa mujibu wa katiba hii watadumu madarakani kwa muda wa miaka mitatu (3), lakini wanaweza kuchaguliwa tena.

           

IBARA YA 25: SIFA ZA KIONGOZI:

                       

25.1     Awe mwanachama wa FENGD

25.2     Awe na uwezo wa uongozi na kupambanua mambo

25.3     Awe mwenye sifa na uwezo wa uongozi

25.4     Mwenye kujituma

25.5     Anaye kubali kutoa na kupokea ushauri toka kwa watu wengine walio wanachama na wasio wanachama wa FENGD na kuufanyia kazi.

25.6     Awe tayari kujitolea kuliko kutegemea mapato/ malipo toka FENGD.

 

IBARA YA 26: KUONDOKA KATIKA UONGOZI:

            Viongozi wanaweza kuondoka madarakani kwa njia zifuatazo;

26.1 Kutokuchaguliwa tena na wanachama

26.2 Kujiuzulu

26.3 Kupigiwa kura ya kutokuwa na imani na wanachama

26.4 Kufukuzwa kutokana na makosa ya kukiuka katiba hii

26.5 Kuhukumiwa kifungo jela kwa makosa ya jinai n.k

26.6 Kupata maradhi ambayo yataathiri kabisa uwezo wake wa kutekeleza majukumu yake ya kila siku.

26.7 Kufariki dunia.

26.8 kuhama makazi ya kudumu nje ya wilaya ya Geita

 

SEHEMU YA TISA:

 

SEHEMU YA IX: MAPATO NA USIMAMIZI WAKE

 

IBARA YA 27: MAPATO, UHIFADHI NA UTOAJI WA FEDHA BENKI:

27.1  Mapato ya FENGD yanatokana na ada za uanachama, ada za kiingilio, michango ya wanachama, ruzuku na misaada ya wafadhili/ wahisani mbalimbali wa FENGD.

27.2 Mwaka wa fedha wa FENGD utaanza tarehe 1 Januari na kuishia tarehe 31 Desemba ya kila mwaka

27.3  Fedha zote za FENGD zitawekwa katika tawi la benki litakalokuwa limeteuliwa isipokuwa fedha za matumizi madogomadogo zisizozidi 50,000/= zitahifadhiwa kwenye ofisi ya FENGD (Kama Petty Cash).

27.4  Waweka saini benki watakuwa wane (4) ambao ni Mwenyekiti, Muhasibu na wajumbe wawili watakao chaguliwa na Bodi yaUshauri ambapo kati yao wawili watakuwa kundi “A”na wawili watakuwa kundi “B”.

27.5  Fedha zitatolewa benki kwa kusainiwa na watu wawili mmoja kutoka kundi A na mmoja kutoka kundi B.

 

 

SEHEMU YA KUMI:

 

SEHEMU YA X: MABADILIKO YA KATIBA, KUVUNJIKA NA LAKIRI YA ASASI.

 

IBARA YA 28: MABADILIKO YA KATIBA, KUVUNJA NA LAKIRI YA ASASI:

 

28.0     Mabadiliko ya Katiba:

28.0.1  Katiba haiwezi kubadilishwa au kufanyiwa marekebisho kwa namna yoyote ile isipokuwa kwa uamuzi utakaokuwa umefikiwa katika Mkutano Mkuu maalumu wa wanachama ambao utahudhuliwa na si chini ya theluthi mbili ya wanachama.

 

28.1     Kuvunjika kwa Asasi

28.1.1 FENGD itafikia ukomo kwa kuvunjika kama uamuzi huo utafikiwa na theluthi mbili ya wanachama waliohudhulia Mkutano Mkuu kupiga kura za kukubali uamuzi huo

28.1.2 Kama Mkutano utaazimia kuvunjika kwa FENGD; Bodi ya Ushauri itafanya utaratibu wa kulipa madeni yote ya FENGD na hatimaye kumilikisha mali za FENGD kwa asasi yenye makao yake mjini Geita na yenye malengo yanayofanana na ya Asasi hii.

 

IBARA YA 29: MUHURI NA NEMBO YA FENGD:

29.1    Kutakuwa na muhuri wa Asasi ambao ni wa duara na ndani yake utasomeka MARAFIKI WA ELIMU (W) GEITA na katikati ya maneno hayo kutakuwa na anuani ya FENGD, S.L.P. 45 GEITA.

 

29.2     Nembo ya FENGD.

29.2.1  Nembo ya utambulisho ya FENGD itakuwa na watu wazima wawili wa jinsia zote walioshikana mikono kuwafunika watoto wawili wa jinsia zote na nyuma ya watoto kutakuwa na kitabu chenye kalamu katikati.

29.2.2  Maana ya kuwa na alama hizi ni kwamba kwa kuwa na elimu; kutakufanya kuona mbali, kuwa na upeo mzuri wa matumizi ya anga, kutumia vyema rasilimali za nchi kavu na baharini kwa manufaa ya Taifa.

29.2.3  Kwenye nembo hiyo kutakuwa na maneno yanayosomeka Mtandao Wa Marafiki Wa Elimu (w) Geita * Friends Of Education Network Geita District (FENGD).

 

SEHEMU YA KUMI NA MOJA

 

SEHEMU YA XI: MENGINEYO:

 

IBARA YA 30: UWEZO WA KUJIUNGA NA TAASISI NYINGINE:

 

30.1     FENGD inaweza kujiunga na Asasi na Taasisi nyingine kwa kadri inavyofaa ili mradi uamuzi wa kujiunga na Taasisi au mitandao utaafikiwa na Bodi na wanachama watapata taarifa hizo kupitia kwenye Mkutano Mkuu.

 

IBARA YA 31 UTATUZI WA MIGOGORO:

31.1    Mgogoro wowote ndani ya FENGD utakaoshindikana kupata usuluhishi ndani ya FENGD, utaamuliwa na wanachama wa FENGD katika Mkutano Mkuu na huo ndio utakuwa na madaraka na maamuzi ya mwisho.

 

UTHIBITISHO:

Sisi ambao majina yetu yameorodheshwa hapa chini na kutiwa saini zetu ndio wanachama waanzilishi wa Asasi ya Marafiki wa Elimu (w) Geita (FENGD) mwaka 2015. Kwa kutambua kuwa jamii inategemea juhudi za watu mbalimbali wenye ushirikiano ili kuleta maendeleo; tumeamua kwa ridhaa yetu kufanya uamuzi wa kuanzisha Asasi hii ambayo itafanya kazi kwa ushirikiano na jamii, wataalam mbalimbali na wadau kutoka serikalini na wadau wanje ili kufikia malengo ya FENGD na maendeleo ya Taifa.

 

Tutailinda, kuiheshimu na kuitunza Katiba hii ili itekeleze majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za kisheria za Tanzania.

 

No
JINA
SAINI
1
 
 
2
 
 
3
 
 
4
 
 
5
 
 
6
 
 
7
 
 
8
 
 
9
 
 
10
 
 
11
 
 
12
 
 
13
 
 
14
 
 
15
 
 

 

 

TUNATHIBITISHA KWAMBA HII NI NAKALA HALISI YA KATIBA YA FENGD

**********************************************************************

 

MUUNDO WA FENGD